Monday, May 24, 2010
WOTE TUFAIDI MAJI YA MTO NILE
TANZANIA ni moja ya nchi zilizosaini mkataba wa ushirikiano wa matumizi endelevu ya Bonde la Mto Nile kati ya nchi 10 zinazotumia rasilimali ya maji katika mto huo.
Wiki iliyopita mawaziri wanaohusika na maji kutoka katika 10 ambazo zinanufaika na maji na rasilimali za Mto Nile walikutana kutia saini makubaliano ambayo yangesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa ukiritimba wa kutumia rasilimali za Mto Nile.
Katika kikao hicho, tunaambiwa ni nchi nane tu ambazo zilisaini makubaliano hayo kati ya nchi 10.
Hata hivyo, ingawa nchi mbili ambazo ni Sudan na Misri hazikusaini makubaliano hayo bado zina nafasi ya kufanya hivyo hadi katikati ya mwaka ujao.
Kwa maoni yetu, makubaliano haya yatasaidia kwa kiasi kikubwa nchi husika kutumia rasilimali za Mto Nile bila upendeleo na kwa uwazi zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.
Tunaamini kwamba hata nchi ambazo zimegoma kusaini makubaliano ya kushirikiana katika matumizi ya Mto Nile zitafanya hivyo kwa manufaa ya Waafrika wote.
Ni vema wenzetu wakaona umuhimu wa nchi ambazo ndio chanzo cha maji ya Mto Nile nao wakaweza kufaidi maji hayo kwa kilimo na hata kuzalisha nishati ya umeme.
Tumeshuhudia maeneo kama Ethiopia na hata mikoa ya Kanda ya Ziwa hapa nchini wakazi wake wakikumbwa na uhaba wa maji ya kutumia, lakini kutokana na sheria za kikoloni ambazo waweka kwamba vyanzo vya maji ya Mto Nile visitumiwe na badala yake wataopaswa kutumia maji hayo ni Misri tu.
Ni kweli Misri hawana njia nyingine ya kupata maji, lakini dawa si kususia kusaini makubaliano ya matumizi ya rasilimali bali ni kukaa pamoja na kuangalia njia za matumizi bora.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment