Monday, May 24, 2010
JIJI KUANZISHA RADIO
HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam, inatarajia kutumia Sh200 milioni, kugharimia ujenzi wa kituo cha radio na televisheni.
Radio hiyo itakayojulikana kama la City Radio, inatarajiwa kuwa katika moja ya vyumba vya jengo la halmashauri hiyo na tayari mkandarasi atakayefanyakazi ya ukarabati ameshapatikana.
Habari zinasema kazi hiyo itakamilika ndani ya kipindi cha wiki sita kuanzia sasa.
Akizungumza wakati Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji lilipotembelea eneo hilo jana, Mkuu wa Kitengo cha Itifaki na Uhusiano wa Umma wa Jiji la Dar es Salaam, Gaston Makwembe, alisema tayari halmashauri imeshapata kibali kutoka Mamalaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kinachoruhusu kuanzishwa kwa kituo hicho.
Makwembe alisema mamlaka kibali hicho ni kwa ajili ya radio tu na si kwa kituo cha televisheni.
Alisema katika hatua hiyo jumla ya Sh 100 milioni zitatumika katika kukarabati ujenzi wa jengo la kituo, kununulia mitambo na vifaa mbalimbali kwa ajili ya radio hiyo.
"Tumeshapewa kibali cha mwaka mmoja kwa ajili ya kukarabati jengo litakalo tumika kwa ajili ya kuanzisha radio ingawa wametupa masharti kuwa kama tutashindwa kutekeleza ndani ya mwaka mmoja, watatunyang'anya masafa,", alisema Makwembe.
Kwa mujibu wa Makwembe, jina lilopendekezwa awali la Bandari ya Salama, halitatumika na badala yake, itaitwa City Radio.
Kwa upande wao madiwani, wamepinga vikali mpango wa kuingia ubia na China katika kuanzisha kituo hicho, kwa maelezo kuwa wanataka kutumia rasilimali za ndani na si za China.
Madiwani hao walisema hawaoni sababau ya kuingia ubia na nchi hiyo kwa kuwa awali nchi hiyo ilitaka kumilikia asilimia kubwa katika vipindi na kurushwa kwa lugha ya Kichina kama ingeingia ubia na jiji.
Mmoja wa wabunge, Charles Keenja alisema haoni sababu ya Jiji kuingia ubia na China kwa sababu hata Tanzania inaweza kuendesha kituo hicho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment