Monday, May 24, 2010
USAFIRI WA PIKIPIKI UTAZAMWE KWA JICHO LA TATU
AJALI za barabarani zinazotokana na uendeshaji wa pikipiki zinazidi kuongezeka kadri siku zinavyosonga mbele huku mamia ya watu wakipoteza maisha na maelfu kupata majeraha makubwa.
Taarifa kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani zinasema kwamba zaidi ya watu 667 wameripotiwa wamekufa na wengine 5,525 wamejeruhiwa vibaya katika ajali za barabarani zilizosababishwa na pikipiki kuanzia mwaka 2008 hadi hivi sasa.
Sababu kubwa ya kutokea kwa ajali hizo imeelezwa kwamba ni uzembe wa waendesha pikipiki kwa kutozingatia taratibu za usafiri huo ikiwemo kutovaa kofia.
Vilevile, taarifa zaidi zinasema kwamba wengi wa waendesha pikipiki hizo hawana leseni na hata hawazitambui sheria za barabarani.
Ni kweli usafiri wa pikipiki unasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza adha ya usafiri hasa maeneo ambayo miundombinu yake ya barabarani si mizuri, lakini hatuwezi kuruhusu maafa kwa watumiaji wa huduma hiyo.
Tunaamini askari wa usalama barabarani wanapaswa kwanza kuhakikisha kwamba wale wote ambao wanaendesha pikipiki hizi wanazingatia sheria za usalama mojawapo ikiwa ni leseni halali na kuvaa kofia kwa abiria na yule anaeendesha.
Mara kwa mara tumeshuhudia pikipiki zikibeba abiria hadi katika maeneo ya mjini, lakini askari wa usalama barabarani wamekuwa hawazikagui na hivyo kuendeleza wimbi la kusababisha ajali.
Vilevile, tunawaasa wale wote ambao wanamiliki vyombo hivi vya usafiri kuhakikisha kwamba wanaajiri waendeshaji ambao wamefuzu vema mafunzo na wawe wenye leseni halali za kuendesha pikipiki.
Ni maoni yetu kwamba kama wamiliki wataajiri watu wenye leseni na wanaojua sheria zinazotawala usafiri wa barabarani basi kasi ya kusababisha vifo itapungua kwa kiasi kikubwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment